Monday, August 16, 2010

Viongozi wa juu wa ccj wahamia chadema

Ikiwa ni miezi mitatu na nusu tangu FREDRICK MPENDAZOE ahamie CCJ kutoka Chama Cha Mapinduzi, CCM kwa madai kuwa chama hicho tawala kinashindwa kutekeleza baadhi ya maamuzi yake, hii leo MPENDAZOE ameondoka CCJ na kuhamia CHADEMA kwa madai kuwa hatoweza kugombea nafasi yoyote ya uongozi kupitia CCJ kwa kile alichoeleza kuwa ni mizengwe katika usajili wake.
MPENDAZOE na viongozi wenzake wengine waandamizi wawili Mwenyekiti wa CCJ Taifa, RICHARD KYABO na Naibu Katibu Mkuu CCJ-Bara, DICKSON NG’HILY wamepokelewa rasmi CHADEMA na mwenyekiti FREEMAN MBOWE.
Katibu Mkuu wa CCJ Renatus Muabhi ambaye amesalia, aliwaponda viongozi waliohama chama hicho na kudai kuwa ni walafi wenye uchu wa madaraka.

Alisema licha ya kuwa viongozi hao wamehama bado kitaendelea kujiendesha kwa malengo kiliyokusudia huku akidai watatangaza nafasi zilizoachwa wazi na viongozi hao ili kuendeleza shughuli zake. Muabhi alisema ameshawasiliana na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, ambaye yuko nje ya nchi ili kuchukua fomu na atakutana na waandishi wa habari kuelezea watakaojaza nafasi hizo.
Alisema kitendo cha viongozi hao kuhama huku wakiwa bado hawajafikia hata chembe ya malengo waliyokuwa wameafikiana, ni sawa na kuendekeza njaa na uchu wa madaraka, ambapo waliona kuwa wasingeweza kuyasubiri kwa muda mrefu wakiwa hapo.
“Hawa wana uchu wa madaraka, haiwezekani katika kipindi cha miezi sita au mitatu, ukahama vyama tofauti zaidi ya viwili au vitatu, hali hiyo kamwe si kuendeleza demokrasia, bali ni uchu mbaya wa madaraka,” alisema Muabhi.

Alisema pamoja na viongozi hao kukimbia chama bado mwelekeo wake uko pale pale na kwamba wanaendelea kujipanga ili kupata usajili wa kudumu kutoka kwa Msajili huku wakiangalia namna ya kwenda na kujiimarisha vijijini. “Hatuwezi kukiua chama kwa sababu ya maslahi ya watu kama hao, kwani si lazima chama kiwe na wabunge ndipo kitambulike, vipo vyama vingapi havina wabunge, lakini vinatambulika kutokana na hoja zao?” alihoji Muabhi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mpendazoe alisema wamekuwa na mazungumzo ya muda mrefu na viongozi wa Chadema kutokana na ukweli kuwa vyama hivyo vina itikadi na mwelekeo unaofanana, ambapo ushirikiano wao ungeendelea baada ya CCJ kupata usajili wa kudumu. Hata hivyo, viongozi hao walipotakiwa kueleza hatma ya CCJ, walisema chama hicho kilikuwa na wanachama wapatao 9,500 na baada ya kuondoka hao watatu, waliobaki takriban 9,497, waulizwe wenyewe watafanya nini, jambo lililoashiria kifo cha chama hicho.

“Sasa kwa kuwa muda tuliobaki nao ni mchache kwa CCJ kupata usajili wa kudumu na kufanya maandalizi ya kutosha kuelekea uchaguzi mkuu ujao, tunatoa mwito kwa wana CCJ wenye sifa na nia ya kugombea uongozi wa kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu ujao wapitie Chadema,” alisema Mpendazoe. Alisema wanafanya hivyo kwa maslahi ya Taifa na si yao binafsi au chama na ndiyo maana wakaamua kuachia nafasi zao na kujiunga Chadema kuwa wanachama wa kawaida.

Hivyo, waliwaomba wanachama wa CCJ waliosalia kuchagua watakaogombea kupitia Chadema, kwani umoja ndiyo nguvu pekee katika kujenga usawa na uhuru katika kuondoa umasikini, ujinga, maradhi na kupambana na ufisadi. Alisema kujiunga Chadema ni mwanzo mzuri kwao kugombea ubunge na udiwani, jambo litakalosaidia wapinzani wengi kupanga maendeleo ya wananchi bungeni na kwenye halmashauri na kuleta mabadiliko makubwa katika uendeshaji wa nchi.

Akizungumzia usajili wa CCJ, Mpendazoe alisema si kweli kuwa Dar es Salaam wana wanachama 13 tu na Pwani hawana mwanachama wala ofisi huku Zanzibar wakiwa na mwanachama mmoja, bali hizo aliziita fitina za Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, baada ya kuona chama hicho kimepokewa vizuri na wanachama wa rika zote. Alisema mpaka sasa kuna Watanzania takribani 9,500 waliojiunga CCJ, wengine wakiwa nje ya nchi kama vile Marekani, Japan, Uingereza, Korea Kusini na Afrika Kusini, ambao walijiunga kwa kufika katika ofisi zao au kushawishiwa na wananchi waliokuwa tayari wamejiunga awali, mbali na wanachama 102 waliojiunga katika mkutano wa kumpokea uliofanyika Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam.

Mpendazoe alisema waliahidi kumpeleka mahakamani Tendwa, lakini hawakufanya hivyo kutokana na kuhofia kuzuiwa chama hicho kufanya jambo lolote, ikiwa ni pamoja na mikutano kwa madai kuwa suala hilo bado liko mahakamani linashughulikiwa. Akiwakaribisha wanachama hao wapya, Mbowe alisema Chadema inaongozwa kwa misingi na utaratibu waliojiwekea wanachama, kwani hakuna ubaguzi wa mwanachama mkongwe au mpya; wote wana haki sawa.

“Si lazima wanachama hawa wapya kurudisha kadi zao za zamani, kwa mujibu wa utaratibu wetu Chadema, mtu anapochukua kadi yetu tunamtambua kuwa ni mwanachama wetu halali,” alisema Mbowe. Alisema si jambo la ajabu kwa viongozi hao kujiunga nao, kwani “siasa haina mwelekeo maalumu, ni sawa na kubadilisha gia pale unapoona kuna maslahi kwa Taifa.”

Aliwataka Watanzania kuacha ushabiki, kwani katika uchaguzi ujao, wana nafasi ya kuliokoa au kuliangamiza Taifa. CCJ ilipata usajili wa muda Machi 2 mwaka huu na kufanyiwa uhakiki kilioulalamikia ambapo Juni 3 ulifanyika Dar es Salaam na kati ya wanachama wake 247 waliokuwa wameorodheshwa, 40 tu ndio waliohakikiwa, 13 wakakosa sifa za uanachama, huku 27 wakibainika kuwa mamluki.

Uhakiki uliofanyika Kibaha, Pwani, Juni 4 haukuona kiongozi, mwanachama wala ofisi ya chama hicho na hivyo Msajili kwenda Morogoro Juni 5 ambako hali ilikuwa vivyo hivyo na hatimaye Zanzibar Juni 9, ambako inadaiwa alipatikana mwanachama mmoja tu na hivyo kukiosa sifa ya kupata usajili wa kudumu. CCJ ilianza kwa nguvu kubwa huku ikijigamba kutumia falsafa ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na wakati fulani uongozi kufanya ziara kwenye kaburi lake kijijini Butiama, Musoma Vijijini, kama njia ya kutafuta baraka zake.

No comments:

Post a Comment