Monday, August 16, 2010

Je, msomi ndiye kiongozi mzuri?







NINAAMINI mojawapo ya makosa tuliyoyafanya baada ya Uhuru na bado tunaendelea kufanya ni kosa la kuhusisha moja kwa moja uongozi na usomi.
Kuna imani ambayo imejengeka kutokana na kosa hilo kuwa kiongozi mzuri ni msomi, na msomi ni kiongozi mzuri.
Katika kongamano la Mwalimu Julius Nyerere siku chache zilizopita Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lile ambalo nimeliandika hapa miezi michache iliyopita limerudiwa japo kwa mbiu kubwa zaidi kuwa tatizo la Afrika (na moja kwa moja Tanzania ) ni uongozi.
Tatizo la bara letu na tatizo kubwa la watu wetu si ukosefu wa fedha, si ukosefu wa watu au rasilimali mbalimbali, na ukifirikia sana utaona tatizo haliko kwenye sayansi na teknolojia. Matatizo tunayoyaona kwenye maeneo hayo ni dalili tu ya lile tatizo kubwa ambalo ni la uongozi. Nimeandika kwa kirefu huko nyuma juu ya hili.
Nilipowasikiliza na kufuatilia mijadala mbalimbali ambayo imekuwa ikifanywa na nikiangalia historia ya jinsi gani tuliwapata viongozi wetu wa awali ambao ni wazalendo, niligundua tatizo jingine ambalo naamini bado hatujatafuta njia iliyo bora ya kulikabili na sidhani katika makala yangu hii fupi nitakuwa na pendekezo la njia hiyo. Kwamba tatizo la uongozi tunaloona dalili zake katika Tanzania kimsingi ni tatizo la mchanganyo wa mambo.
Ukiondoa viongozi wachache tuliowapata kwenye taasisi mbalimbali za umma na idara mbalimbali baada ya Uhuru na hata baada ya Muungano utaona kuwa “usomi” ilikuwa ni sifa moja kubwa. Kutokana na kutukuza hadhi hii ya usomi naamini kuna mahali tulipotea na kuwaacha viongozi wazuri kwa sababu hawakuwa wamesoma sana.
Hivyo, tukafika mahali ambapo hata katika maeneo ambayo hayahusiani na fani ya mtu au hayahitaji utaalamu maalumu tulihakikisha kuwa mtu anayeshika nafasi hiyo basi anakuwa amesoma kwa namna fulani.
Matokeo yake “usomi” ukaanza kututengenezea kasumba ya aina fulani, kasumba ya kumdharau asiyesoma hadi kufika chuo kikuu, na kama mtu amefika chuo kikuu basi kumheshimu zaidi yule aliyeweza kupata shahada za juu zaidi na ambaye anaweza kutuonyesha katika wasifu wake wa kisomi ni mambo gani ya kisomi ameyafanya na vitabu gani ameandika.
Hivyo, tukajikuta unapotokea uchaguzi kitu cha kwanza tunachoangalia ni je, mtu huyu anasema amesoma kwa kiasi gani na kama mbele ya jina lake kuna herufi za “Dk” basi mtu huyo anakuwa na ujiko kuliko wa mtu yule ambaye hana herufi hizo. Na hata yule ambaye hana “Dk.” tunaangalia kama mwisho wa majina yake ameongeza “B.A, BS, M.A, au M.Sc na vingine”.
Hivyo, tukaendeleza hili kosa la kuamini kuwa msomi ndiye kiongozi bora na kuwa tukitaka kumjua kiongozi bora tuangalie kama ni msomi.
Na katika kuangalia usomi huo tukaingia kwenye mtego ule ambao ulitegeuza kwa kiasi fulani kuwaona wazee wetu wasiosoma kuwa ni duni; mtego wa kupima elimu na kuelemika kwa kuangalia karatasi! Kwamba, tunamuita msomi mtu ambaye amepata elimu rasmi kutoka katika vyuo vikuu vya kitaaluma na yule ambaye ana utaalamu wa kujifunza kutokana na uzoefu wa muda mrefu au kufundishwa pasipo kupewa karatasi la kuhitimu basi anaonekana si “msomi”.
Hili lilionekana hasa katika sehemu ambazo zinahitaji ufundi ambapo mhitimu mwenye cheti anafika mahali na anashindwa kufanya mambo kwa mujibu wa “kitabu” na anajikuta anakwama lakini mzee mmoja ambaye amejifunza katika darasa la “shule ya kazi ngumu” akapendendeza njia zilizojaribiwa kwa muda mrefu na akatoa suluhisho ambalo kijana wetu hakujifunza katika vitabu vya Fizikia, Kemia na Hisabati!
Sasa mzee ambaye hana elimu ya namna hiyo lakini anajua anachofanya kwani amekifanya kwa muda mrefu atajikuta analipwa fedha kidogo kulinganisha na msomi wetu. Matokeo yake kumekuwa na ile hali ya uadui  katika baadhi ya maeneo ya kazi, wale wakongwe wa kazi wasio na vyeti vya vyuo vikuu wanajikuta wanatumika kufanya mambo ambayo “msomi” wetu ndiye anapewa sifa.
Nakumbuka tulifika mahali (sijui kama tuliondoka) ambapo maofisa wa Polisi waliokaa jeshini kwa muda mrefu na wamejifunza kazi ya upolisi kwa vitendo na wamekuwa waaminifu wanajikuta hawapandi vyeo kwa haraka au kwa jinsi wanavyostahili, kisa tu kuwa walipoingia waliingia wakiwa na elimu ya darasa la saba. Licha ya ukweli kwamba maafisa hao wanafanya kazi nzuri zaidi ya kulinda jamii na kutoa ushauri wa jinsi gani ya kupambana na genge la majambazi.
Kinachowaumiza ni kuwa kijana aliyemaliza kidato cha sita au digrii ya kwanza anaingia jeshini na baada ya miezi michache anaanza na “kanyota” kamoja!
Ubaya zaidi ambao naamini umetuumiza sana ni kuwa mawazo haya ya kikoloni ya kutukuza usomi wa makaratasi na si uwezo wa kuongoza yametufikisha mahali pa kuamua viongozi wetu wa kitaifa kuwa ni wale ambao tunaamini “wamesoma”. Matokeo yake ni kuwa na wezi wakubwa wa mali zetu, waliotuingiza kwenye mikataba mibovu, walioidumaza Tanzania ambao ndio tunaowaita “wasomi”!
Walioandika sheria zetu ambazo nyingine huwa najiuliza waliziandika wakiwa wamelala? Na wale ambao wamewekwa kusimamia sheria hizo utakuta ni wasomi waliokubuhu na wengine wanatanguliwa na cheo cha “uprofesa”!
Sasa, bila ya shaka unaweza ukafikiria ninabeza usomi au nakejeli watu waliosoma. La hasha! Ninakwenda mbali zaidi. Ninaamini, kumpima kiongozi mzuri kwa kuangalia usomi wake ni makosa makubwa ambayo yanapaswa tuyarekebishe. Kwani, kwa kufanya hivyo tumefikia mahali tuna mawaziri wenye digrii feki tena wakishika nyadhifa nyeti na hakuna mtu anayeona tatizo hilo! Ikulu wamelikubali, Bunge wamekubali na wao wenyewe wamekubaliana kuitana “madokta”!
Tumefika mahali watu wako tayari kufanya lolote wanaloweza kufanya ili tu na wenyewe waonekane wamesoma (kwenye makaratasi).
Ndiyo maana mimi binafsi bado naamini kile kipimo cha Mwalimu Nyerere kuhusu usomi kuwa “elimu imsaidie mtu kuyakabili mazingira yake”. Msomi wa kweli basi si mtu ambaye anajivunia au anaonyesha ni kwa kiasi gani amepata elimu bali ni mtu ambaye kutokana na elimu aliyoipata anapendekeza njia bora za kukabiliana na mazingira na matatizo yetu, na si tu anazipendekeza njia hizo bali pia anazitendea kazi ili mtu ambaye hajasoma aweze kuelewa na kushawishika kuwa ipo njia bora ya kufanya jambo.
Kwa mfano, mahali ambapo pana mto ambao si mpana sana na kina chake cha maji ni kirefu na zipo jamii pande mbili za mto huyo je watu wafanye nini ili kuvuka. Njia ya kawaida ni kutumia mtumbwi au kujenga darala la kamba. Mtu msomi ambaye amejifunza uhandisi anaweza akaliangalia eneo lile na kujenga hoja kuwa kutokana na vitu mbalimbali vilivyopo pale wanaweza kutengeneza daraja ambalo linaweza kuvusha watu na mizigo bila kutumia gharama nyingi sana.
Msomi huyo anaweza akawashawishi wasomi wenzake na kwa pamoja wakaweza kuishawishi jamii kubwa kufanya jambo hilo. Tatizo letu ninalilona ni kuwa msomi wetu wa leo hii atakachofanya ni kuangalia jinsi gani “wafadhili” watajitokeza kufadhili mradi huo huku akifikiria ni mgao wa kiasi gani atauhitaji ili kumalizia kibanda chake! Msomi wetu wa leo anaweza kujikuta anaogopa kutoa pendekezo hilo kwani ataonekana anajifanya anajua sana!
Ukweli ni kuwa hatuwezi kuwapima viongozi wetu kwa kuangalia elimu yao tu. Usomi wa kweli wa mtu hauonekani kwa kutamba kuwa yeye ni “msomi” na ya kuwa “kasoma” sana. Msomi wa kweli si yule ambaye anajivunia kuhitimu chuo kikuu na sifa kibao bali ni mtu yule ambaye kutokana na elimu yake hiyo ameweza kushughulikia matatizo fulani au suala fulani na kusababisha kulifanya kuwa rahisi, kuliondoa au kuhakikisha kuwa linabadilishwa kwa kiasi kinachostahili.
Hivyo basi utaona kuwa viongozi wazuri wakati mwingine si wale walio wasomi wakubwa! Hapa ndipo haja ya kutafuta kipimo kipya na cha uhakika zaidi cha kiongozi bora inapokuja. Je, kiongozi mzuri tunaweza kumtambua vipi? Na tukimtambua tunawezaje kumpima na kujua kuwa ni bora kuliko wengine? Je, kiongozi huyo tunauhakika gani akiingia madarakani hatabadilika kuwa fisadi?
Tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwakani na hata wa Mitaa baadaye mwaka huu, hatuna budi kufikiria vipimo vipya vya kiongozi bora. Je, tumchague mtu na kuwa kiongozi kwa sababu tu ya usomi wake bila ya kuangalia rekodi yake ya kazi? Je, ni kwa kiasi gani historia ya kazi, mafanikio, na umahiri wa utendaji vinatakiwa kuonyeshwa kwenye wasifu wa mgombea?
Kwa mfano ukimuona mgombea ambaye anasema “Mimi  Juma Peter nimesoma Chuo Kikuu cha Dar na kupata Shahada ya kwanza katika Sheria, ninazungumza Kireno na Kijerumani, nimesomea pia uhandisi huko Ujerumani ambako nilipata shahada yangu ya Uzamili, na pia sasa hivi namalizia shahada yangu ya Udaktari katika mambo ya Fizikia  kutoka Uingereza” na mwingine mgombea kwenye uchaguzi wa nafasi hiyo hiyo anajiita Esther Bakari ambaye anasema “Nimesoma hadi kidato cha nne, nina uzoefu wa miaka 20 katika kazi mbalimbali. Nimeweza kubuni na kuendesha kampuni yangu binafsi ambayo nilianza na mtaji wa shilingi 100,000 na sasa mtaji wangu wa kazi unafikia shilingi milioni 50. Nilipoanza kufuga kuku ilikuwa ni biashara yangu  binafsi lakini sasa nimeweza kuanzisha kampuni ya kutotolesha vifaranga ambapo nimetoa ajira kwa vijana 50, na kutoka na uzoefu wangu wa biashara mbalimbali nimefungua kituo cha mafunzo kwa wasiojiweza ambapo kila mwezi vijana wapatao 30 wanapata mafunzo ya mambo mbalimbali ya biashara”.
Je, wewe kama mpiga kura ni yupi unaamini anadokeza sifa za kiongozi mzuri? Binafsi ningempenda Esther na kumchagua kwani kuna kipimo naweza kukiona cha uongozi wake.
Hata hivyo, Watanzania wengi hatupigi kura kwa mambo hayo na vyombo vyetu vya habari haviwachambui wagombea wetu kwa mtindo huo. Mgombea akisema yeye ni msomi basi ni usomi wake unaotukuzwa na rekodi yake ya utendaji wake wa kazi inawekwa pembeni.
Matokeo yake tumeendelea kuwarudisha bungeni maprofesa walioshindwa kuongoza na tumewazawadia uwaziri watu wasiostahili kwa sababu tu wanavyeo vya udaktari.
Ninaamini hata hivyo kuwa, kinadharia msomi ambaye amejifunza na kubobea katika fani fulani angekuwa ni kiongozi mzuri wa mfano. Kinadharia mtu ambaye amejifunza mambo fulani kwa kina na akayaongeza kwenye uzoefu wake basi anakuwa na sifa kubwa zaidi za kiongozi bora. Yaani, si tu usomi wake anaojivunia bali ana kitu cha kuonyesha kuwa ule usomi alionao umemsaidia kuyakabili mazingira yake na ameweza kuisadia jamii yake kukabiliana na matatizo mbalimbali na kuonesha njia bora za kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Hivyo, kiongozi ambaye ni msomi ni chachu kubwa zaidi ya maendeleo. Tatizo letu litakuwa ni jinsi gani tutampata mtu wa namna hiyo? Je, ni kipi kiwe kigezo cha mwisho cha kumchagua mtu kati ya elimu yake na uzoefu wake wa kazi?
Tukiendelea kuangalia elimu tu na kuiweka juu ya vigezo vingine tutakuwa tunarudia kosa tulilolifanya baada ya Uhuru, tulilolirudia miaka na miaka na ambalo bado tunaliendelea kulifanya. Nalo, ni kufikiria uongozi ni usomi  na kuwa msomi ndiye kiongozi bora.
Ni lazima tufikirie namna mpya, ya uhakika zaidi, iliyo bora zaidi ambayo itachukua yote mawili (usomi na uzoefu) na vikolombwezo vingine na kutengeneza kipimo (matrix) kilichobora zaidi cha kiongozi. Ili hatimaye, tuondokane na viongozi uchwara ambao sifa yao iko kwenye makaratasi na uwezo wao uko kwenye kujisifia.
Ni lazima tufikirie ni jinsi gani tutapata viongozi wazalendo, wenye moyo wa kujituma, ambao ni mfano bora na ambao wana uwezo wa kutuongoza kutoka hapa tulipo kuelekea mafanikio ya kweli.

No comments:

Post a Comment